Home » » NAMNA YA KUPATA TIN NAMBA YA KAMPUNI,NGOs NA VIKUNDI/SACCOS.
NAMNA YA KUPATA TIN NAMBA YA KAMPUNI,NGOs NA VIKUNDI/SACCOS.
NA BASHIR YAKUB -
Nilipoandika kuhusu namna ya kuunda kampuni nilieleza pia kuwa unapokuwa umekamilisha usajili wa kampuni na umepata cheti cha usajili yapo mambo mengine ya kufanya kabla ya kuanza rasmi biashara. Moja ya mambo hayo nilisema ukishapata cheti unatakiwa uende manispaa husika ukapate leseni ya biashara. Manispaa husika ni manispaa ambako ofisi ya kampuni yako itakuwa. Kitu kingine baada ya kupata cheti cha usajili ni kupata namba ya mlipa kodi (TIN). Ili kampuni ifanye biashara kisheria inatakiwa kuwa imepata namba hii.
Yawezekana wanahisa kila mmoja anayo namba yake ya mlipa kodi lakini namba hizo haziwezi kutumika kwakuwa ni za watu binafsi na si za kampuni. Kampuni inatakiwa ipate namba yake inayojitegemea.
Halikadhalika kwa wanaoanzisha vikundi kwa mfano saccos, na asasi za kiraia( NGOs) nao wanatakiwa kuwa na namba ya mlipa kodi ya vikundi hivyo.
1.TIN NAMBA HUPATIKANA WAPI.
Mamlaka ya mapato Tanzania ( TRA) ndiyo mamlaka inayoshughulika na utoaji wa namba za mlipa kodi. Awali namba hizi zilikuwa zikitolewa makao makuu ya mamlaka ya mapato ambapo kwasasa katika kuboresha huduma wameweka ofisi za kikanda sehemu mbalimbali ambazo huhudumia wahitaji wa kanda husika kwa mfano kwa Dar es salaam eneo la ilala , buguruni, tabata, kariakoo ofisi zipo makutano ya Shaurimoyo badala ya mnazi mmoja au samora . Hata hivyo yapo maeneo mengine ambayo ofisi za kanda hazijawekwa kwa mfano mikoani ambapo wahitaji hulazimika kufuata huduma hii makao makuu ya mamlaka ya mapato.
2. KUPATA TIN NAMBA YA KAMPUNI.
Ili kupata TIN namba ya kampuni unahitaji kwenda na viambatanisho vifuatavyo.
( a ) Picha mbili za passportsize kwa kila mkurugenzi. Wakurugenzi wawe wawili, watatu au mmoja kila mmoja atatakiwa kuwasilisha picha zake mbili.
( b ) Nakala moja ya kitambulisho kwa kila mkurugenzi. Hapa kitambulisho kinaweza kuwa cha taifa, cha mpiga kura, cheti cha kuzaliwa, hati ya kusafiria au leseni ya kuendeshea.
( c ) Nakala moja ya katiba na waraka kampuni( memorandum & article of association). Hii ina lengo la kuonesha aina ya biashara ambazo kampuni itakuwa inazifanya.
( d ) Nakala moja ya cheti cha kuzaliwa kwa kampuni( certificate of incorporation). Hii ni kuthibitisha kuwa kampuni inayoomba namba ya mlipa kodi imesajiliwa kisheria.
( e ) Mkataba wa pango wa eneo ambalo biashara itakuwa ikifanyika. Kama ni nyumba yako basi utawasilisha nyaraka ya umiliki wa nyumba iyo.
( f ) Barua iliyojazwa na mwenyekiti wa serikali za mitaa wa eneo ambalo biashara itafanyika. Barua hii hutolewa na mamlaka ya mapato TRA na hujazwa na mwenyekiti wa serikali za mitaa. Kwahiyo barua hii utaifuata TRA na kuipeleka seriklali za mitaa ili ikajazwe na kugongwa mhuri.
Mwisho unapokuwa umekamilisha viambata hivi utaenda TRA ambako utakuta fomu maalum utazotakiwa kujaza. Katika fomu hizo kuna sehemu wakurugenzi wa kampuni watasaini pamoja na mwenye nyumba wako aliyekupangisha ofisi kama umepanga. Baada ya hapo utafanyiwa usaili( interview) kwa ajili ya kupata namba ya mlipa kodi (TIN ).
3. KUPATA TIN NAMBA YA NGOs, VIKUNDI/SACCOS.
Vifuatavyo ni viambatanisho vinavyotakiwa.
( a ) Nakala moja ya cheti cha usajili wa kikundi kutoka RITA. Mamlaka ya RITA ndiyo hushughulika na usajili wa vikundi na hivyo cheti chao hutakiwa kuambatanishwa ili kuthibitisha usajili.
( b ) Nakala moja ya Katiba ya kikundi na muhtasari wa kikao cha mwisho.
( c ) Picha mbili za passportsize za katibu, mweka hazina na mwenyekiti. Kila mmoja mbili mbili.
( d ) Nakala moja ya mkataba wa pango iwapo ofisi za kikundi zimepangwa au hati, leseni ya makazi, ofa iwapo ofisi sio za kupanga.
( e ) Nakala moja ya kitambulisho kwa kila mbia(partner). Hapa kitambulisho kinaweza kuwa cha taifa, cha mpiga kura, cheti cha kuzaliwa, hati ya kusafiria au leseni ya kuendeshea.
( f ) Barua iliyojazwa na mwenyekiti wa serikali za mitaa wa eneo ambalo biashara itafanyika. Barua hii hutolewa na mamlaka ya mapato TRA na hujazwa na mwenyekiti. Kwahiyo barua hii utaifuata TRA na kuipeleka serikali za mitaa ili ikajazwe na kugongwa mhuri.
Hapa pia baada ya kukamilisha viambata vyote zitajazwa fomu maalum zilizopo mamlaka ya mapato na utafanyika usaili mfupi kwa wahusika na TIN namba itapatikana.
Blogger Comment