Lowassa Atamba Watashinda Uchaguzi asubuhi Oktoba 25......Atoa ONYO Kwa CCM Kuhusu Wizi wa Kura


Mkutano Mkuu wa Chadema, kwa kauli moja, jana umempitisha waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa kuwa mgombea wake wa urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25.
  
Akihutubia mkutano huo mkuu wa Chadema kwa mara ya kwanza, Lowassa alisema chama hicho kupitia Ukawa kitachukua nchi mapema asubuhi Oktoba 25.

Alisema Watanzania wanajua kuwa Chadema wamepania, wamejipanga na wana uhakika wa kukamata dola mwaka huu.

“Nilianza na safari ya matumaini, lakini sasa nasema hii ni Safari ya Mabadiliko nje ya CCM, tutakamata nchi mapema kabisa asubuhi,”alisema Lowassa.

Hata hivyo, Lowassa alitahadharisha kuwa kuing’oa CCM ni kazi kubwa kama hakutakuwa na mipango na malengo huku akisema hakujiunga na chama hicho akiwaza kushindwa na kwamba hana msamiati wa kushindwa na wala hakwenda kwa bahati mbaya, bali alijiridhisha na kukubaliana na familia yake hadi kufikia uamuzi huo.

“Nimekuja Chadema nikijua kuwa kazi ya chama ni kushika dola na kama si hivyo, hakuna sababu ya kuwa chama, nimejiandaa vizuri kushika dola… watu wanasema Chadema haiwezi, Tanu ilipewa nchi ikiwa na miaka saba, sasa ninyi mna miaka 23,” alisema na kushangiliwa.

Aliongeza,“Najua kazi ni kubwa na mnajitolea, ndiyo maana chama kina nguvu na moyo kama CCM ya zamani si ya sasa, ndiyo maana tumeikimbia,” alisema Lowassa.

Alisema atapita kila jimbo kutengeneza mipango ya ushindi kwa kufanya kampeni za kistaarabu huku akionya... “Mradi wasiibe kura zetu.”

Mgombea mwenza, Duni Haji aliirushia kijembe CCM kuwa inafanya wananchi wawe maskini ili iendelee kuwatawala.

Akizungumza baada ya kuteuliwa na chama hicho kuwa mgombea mwenza, Duni alisema, CCM haiwezi kuwasaidia wananchi kutoka kwenye umaskini kwa sababu sera yao ni umaskini.

“Miaka ya 70 hatukuwa na neno changudoa, jambazi wala panya road. Haya yamekuja kutokana na kushindwa kwa utawala wa CCM. Ukawa tumedhamiria kuchukua madaraka ya nchi hii ili kuleta mabadiliko,”alisema.

Alisema wananchi wamejenga imani na matumaini kwa makubaliano yaliyofanyika jangwani, walipotia saini hati ya makubaliano inayoruhusu vyama kukubaliana kusimamisha mgombea mmoja kwenye kila nafasi ya uongozi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Akimzungumzia mgombea urais, Duni alisema: “Siyo jambo rahisi kufanya uamuzi mgumu kama aliofanya Lowassa. Wengi bado wapo CCM licha ya kuwa hawapendi mfumo wa chama chao, alichokifanya Lowassa ni ujasiri mkubwa.”

Hata kwake, alisema halikuwa jambo rahisi kuihama CUF na kujiunga na Chadema. Alisema kuwa alikubaliana na viongozi wake, Profesa Lipumba na Maalim Seif Sharif Hamad aende Chadema ili Ukawa ilete ukombozi katika Taifa.

“Profesa Lipumba ananipenda sana na ananikubali haswa… na anajua kuwa hiki ni kifaa. Lakini alikubali nijivue uanachama wa CUF ili niende Chadema kuongeza nguvu ya kuleta mabadiliko, nina imani Ukawa tutashika dola ifikapo Oktoba 25,” alisema.

Alisisitiza kuwa Ukawa ndiyo ufumbuzi wa matatizo ya Watanzania akisema umoja huo unaungwa mkono na wananchi wengi, hivyo hana shaka kwamba utashinda katika uchaguzi ujao.

“Nilikuwa mwanachama wa ASP nilipokuwa kidato cha pili. Nilipoona mambo yanabadilika nami nilibadilika. Lengo kuu la kupigania uhuru lilikuwa ni Mwafrika kumtawala Mwafrika mwenzake ili amlinde, lakini lengo hilo sasa limepotea.

“Ninashangaa kuona askari wa kimaskini aliyepewa bunduki kuwalinda wananchi, anageuka na kuwapiga risasi maskini wenzake, huu ni udhalimu uliotengenezwa na Chama cha Mapinduzi,” alisema.
Share on Google Plus

    Blogger Comment