CHADEMA Wachangisha Milioni 97 za Kampeni...... Mbowe Asema Wako Matajiri Watano Ambao Wameapa Kukipigania Chama


Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema chama chake kina watu watano wenye uwezo wa kiuchumi wanaoweza kukisaidia chama hicho kuendesha shughuli zake za kampeni, ikiwa ni siku 32 kabla ya wananchi kupiga kura Oktoba 25.

Lakini mwenyekiti huyo wa Chadema amesema watu hao hawataki kutangazwa majina yao kutokana na kuhofia kufuatiliwa na vyombo vya dola, akisema kitendo hicho ni cha kushangaza kwa nchi huru kama Tanzania.

Chadema, ambayo inashirikiana na NLD, CUF na NCCR Mageuzi chini ya mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) iliandaa harambee hiyo juzi kwenye ukumbi wa Mlimani City kwa ajili ya kutafuta fedha za kuchangia shughuli zao za kampeni zinazoendelea kote nchini.

Katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na takriban watu 800, jumla ya Sh97 milioni zilikusanywa, ikiwa ni fedha taslimu, michango kwa njia ya simu na ahadi.

Baada ya kazi ya uchangishaji kuanza, Mbowe alishika kipaza sauti na kueleza michango mingine kutoka nje ya ukumbi huo.

“Wakati tunaendelea na uchangiaji hapa, nimepokea simu kutoka kwa rafiki zangu watano wenye uwezo mkubwa kiuchumi. Wameahidi kuchangia harambee lakini wanaogopa kujulikana kwa kuhofia mkono wa serikali,” alisema mwenyekiti huyo.

“Inasikitisha Mtanzania mwenye uhuru ndani ya Taifa lake anahofia kuchangia safari ya mabadiliko kwa sababu ya kuiogopa Serikali, wakati Serikali iliyopo imejaa mafisadi wakubwa?

“Unaweza kuona hii ni Serikali ya namna gani, lakini ningewaomba niwatie moyo tu ndugu zangu wenye nia ya mabadiliko, tuwe na ujasiri, msiogope.”

Sheria ya Gharama za Uchaguzi, ambayo mwaka huu imeweka kiwango cha juu cha matumizi ya kila chama kuwa Sh17 bilioni, inataka uwazi wa vyanzo vya mapato na matumizi, lakini ni nadra kwa wafanyabiashara kuweka bayana michango yao kwa vyama vya upinzani.

Chadema imekuwa ikinufaika na michango ya fedha na mali kutoka kwa mfanyabiashara maarufu nchini, Mustapha Sabodo, ambaye amekuwa akitangaza hadharani kila anapokichangia chama hicho.

Alipoulizwa ni kiasi gani chama hicho kimepanga kutumia kwenye uchaguzi, Mbowe alisema ni vigumu kutaja.

“Uchaguzi ni dynamic (unabadilikabadilika). Hesabu za siku haziwezi kuwa sawa wakati wote. Kwa mfano bango la kupinga bao la mkono, inahitajika sana kwa wakati huu lakini gharama inaweza kuwa nyingine wakati wa kusambaza bango jingine,” alisema Mbowe.

Mkurugenzi wa mipango na uchaguzi wa CUF, Shaweji Mketo alisema kila chama ndani ya umoja huo kinajitegemea kwenye gharama za wagombea wake kwa ngazi ya majimbo na udiwani.

“Hakuna tathmini ya pamoja ya Ukawa...taarifa za gharama kwa CUF tutaziweka wazi baada ya kukamilisha majumuisho ya taarifa zote kutoka majimboni na ngazi ya madiwani,” alisema Mketo.

Akifungua harambee hiyo, Mbowe alisema mikoa iliyosalia ni mingi kwa hivyo bado wanategemea zaidi michango ya wadau katika kufanikisha kampeni.

Mbowe alisema muda uliobakia ni wa “vita ya lala salama”, ambayo inahitaji bajeti ya kutosha ili kufanikisha kufikia wapiga kura wengi watakaoshiriki uchaguzi huo.

“Ukichangia harambee hii hautakuwa umemchangia Mbowe au Lowassa, bali utakuwa umechangia ufanikishaji wa kufikia ndoto ya mabadiliko. Utakuwa umechangia ukombozi wa akina mama na vijana wa Taifa la Tanzania,” alisema Mbowe.

“Tangu kuanza kwa kampeni hizi, Ukawa tumekuwa tukisaidiwa na Watanzania mbalimbali wenye nafasi zao, wapo waliotoa usafiri wa magari ya kufanyia kampeni. Kwa hivyo tunahitaji sana mchango wako katika kipindi hiki.”

Chadema pamoja na Ukawa zimekuwa zikipambana sambamba na CCM kwenye kampeni za urais na ubunge na matumizi yao makubwa yanaonekana kuwa katika gharama za safari za wagombea, matangazo ya redio na televisheni, matangazo ya moja kwa moja ya mikutano yao ya kampeni, posho za mawakala na vifaa kama mavazi, bendera, vipeperushi na mabango.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, mwenyekiti mwenza wa Ukawa, James Mbatia, ambaye ni pia ni mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, aliwataka waalikwa kuhakikisha wanashiriki kikamilifu kuchangia harakati za mabadiliko ili kufanikisha ndoto za kuwakomboa Watanzania kutoka mikononi mwa Serikali ya CCM.

Mwingine aliyezungumza na waalikwa ni mgombea mwenza wa urais, Juma Duni Haji, maarufu kwa jina la Babu Duni, ambaye alikuwa kivutio kutokana na vijembe na misemo anayotoa wakati akiwa jukwani.


Duni alisema kutoa ni moyo na siyo utajiri kwani wapo wenye fedha nyingi, lakini hawana moyo wa utoaji.
Share on Google Plus

    Blogger Comment