Wapiga Kura Wamtaka Rais Mkapa Awaombe Radhi kwa Kuwatukana


MUUNGANO wa wapiga kura Tanzania (TANVU), umeiomba Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kumchukulia hatua, Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa, kwa kitendo alichokifanya kuvitukana vyama vya upinzani kwa kuwaita viongozi na wanachama wake malofa, vibaka na wapumbavu.

Kauli ya TANVU inakuja ikiwa ni siku chache baada ya Mkapa kutoa maneno ya kuvihadaa vyama vya upinzani wakati Chama cha Mapinduzi (CCM) kilipokuwa kinazindua kampeni za uchaguzi mkuu uliofanyika kwenye viwanja vya Jangwani, Dar es Salaam.

Pia muungano huo umekipatia CCM muda wa siku saba kuanzia leo kuwaomba radhi watanzania kwa kutumia Shirikisho la vyama vya watu wenye ulemavu nchini (SHIVYAWATA) kwenye uzinduzi wa kampeni hizo huku kikitambua ni makosa kisheria kwa vyama vya siasa kutumia Taasisi zisizokuwa za serikali kwenye kampeni za uchaguzi.

Kauli hiyo ya TANVU imetolewa leo jijini Mwanza na Rais wake, Militon Lutabanana wakati akizungumza na wandishi juu ya hali ya kisiasa nchini, demokrasia na kuelekea kwenye uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Amesema hatua ya SHIVYAWATA kushiriki kwenye uzinduzi wa kampeni za kisiasa za CCM ni makosa kwa kuwa kwa mujibu wa sheria za nchi taasisi yoyote isiyo ya serikali hairuhusiwi   kujiingiza kwenye shughuli za kisiasa.

“Kwa kitendo hicho wote wanamakosa CCM na SHIVYAWATA lakini kama CCM haitaomba radhi tutatoa tamko lingine ambalo sisi kama muungano wa wapiga kura nchini hatupendi tufike huko,” amesema na kuongeza.

“Tunaiomba Tume ya Taifa ya Uchaguzi itende haki kwa kumchukulia hatua stahiki Rais Mkapa kama ambavyo jana tumeshuhudia aliyewahi kuwa waziri wa mambo ya ndani ya nchi Laurence Masha alivyoshughulikiwa,” amesema.

Amesema wapiga kura hawahitaji kusikia matusi wala vijembe kutoka kwa wagombea, viongozi au wanachama wa vyama vya siasa wanachotaka kusikia ni sera za vyama hivyo vya siasa na sio vinginevyo.

“Tunawaomba makada wa CCM waache kuendesha kampeni kwa mabavu, Magufuli (John) hatuna tatizo naye tunamshauri asikubali kuombewa kura na watu wanaotumia matusi,” amesema.

Aliongeza kuwa kitendo cha Rais Mkapa kutoa lugha za matusi kitamharibia mgombea wa CCM na kumpunguzia idadi ya kura kwa kuwa yeye alikuwa kama mdhamini wake kwa wapiga kura.
Share on Google Plus

    Blogger Comment